Hatimaye timu ya Tusker ya Kenya imeibuka ni mabingwa wa kombe la Kagame. Ni ushindi ambao umesisimua kwani wengi wa mashabiki walitarajia URA kushinda mechi ile. Kwa kweli mechi hiyo ilikuwa nzuri na iliyojaa ushindani japo URA walijisahau kwa kupoteza umakini katika dakika za mwishoni na kuruhusu wapinzani wao kujipatia mabao mawili ya haraka.
Kwa ufupi mashindano ya Kagame mwaka huu yalikuwa mazuri kwani naamini yaliandaliwa vizuri na kisasa kabisa. Kwanza yalichezwa katika kiwanja kizuri na pia nilishuhudia timu zikitumia vifaa bora vyenye nembo ya wadhamini. Si hayo tu, kila baada ya mechi kulikuwa kuna nafasi ya makocha kufanya mahojiano na wanahabari kitu ambacho kilitia hadhi ya mashindano na kuonesha angalau sasa ukanda wa Cecafa umeanza kujua nini kinatakiwa kifanyike katika kuandaa na kusimamia mashindano.
Kuna mambo kadhaa ambayo napenda niyatathmini kutokana na michuano ya mwaka huu. Moja, vilabu vyetu vikuu ndio chanzo cha kudumaza soka la Tanzania. Navisemea Simba na Yanga kwani utaona vilabu hivi vinawekeza fedha nyingi sana kununua wachezaji kutoka nje ambao viwango vyao ni sawa kabisa na wachezaji tulionao hapa. Sioni mantiki kununua wachezaji kutoka nchi jirani wakati vipaji tunavyo hapa nchini ila tatizo watu hawaishi Dar es salaam. Naamini kabisa nchi hii ni kubwa na ina uwezo wa kupata wachezaji wa kila nafasi.
Pili, pamoja na timu hizi kuwa na walimu kutoka Ulaya lakini bado utaona staili ya uchezaji si ile ambayo mtu ungetegemea wachezaji wetu waioneshe. Sioni jambo jipya hasa kwenye eneo la ufundi na mbinu (techniques). Utaona kabisa kwa mfano Simba ina uwezo mkubwa sana wa kucheza mpira mzuri wa kuonekana lakini hawana mbinu hata kidogo. Yanga nayo ndiyo basi huoni mbinu miongoni mwa wachezaji. Timu zote hizi mbili zinatumia zaidi mpira wa kiasili (traditional football) yaani kila mtu kucheza kwa namba na wala si kwa idara kama mpira unavyochezwa siku hizi. Ni mpira wa aina hii ambao hata Timu ya Taifa, ya Maximo mambo ndio hayahaya.
Tatu, ni hii habari ya mechi ya mshindi wa tatu, ambapo timu ya Yanga iligoma kufika kiwanjani kwa ubishani nadhani wa mgawanyo wa mapato. Ni fedheha kubwa kuwahi kulikumba soka la bongo. Mimi si shabiki wa timu hizi za Dar es salaam, ila siku ile Yanga walipogoma kufika uwanjani nilichukia sana na kujiona ni jinsi gani Tanzania kama nchi imefilisika kifikra. Yaani bila aibu, timu inaamua kujitoa mashindanoni baada ya kushindwa kukubaliana kifedha.
Hali hii ya Yanga kujitoa inanifanya nijiulize hivi kunani TFF? Umefika wakati maandalizi ya mashindano yawe na sheria kali na yasizipe nafasi timu fulani kuwa na sauti ya kimaamuzi juu ya suala la mgawanyo. Mambo yote yawekwe wazi kabla michuano haijaanza. Inakuwaje wakati michuano inaendelea katikati ndio makubaliano juu ya mapato yanafanyika? Hebu tuchukulie kwa mfano fainali iliyopita ya Kombe la Mabingwa Ulaya (Champions League) kati ya Manchester United na Chelsea. Fainali ya timu hizi mbili ilikuwa ni mojawapo ya mechi ambayo ingevutia watu wengi lakini hatukusikia UEFA wakianza kuvutana na vilabu hivi vikubwa vyenye mashabiki lukuki ulimwenguni. Hii ni kwasababu mwanzoni mwa michuano mambo yote yanakuwa yameshaamuliwa kwa mantiki ya kuzingatia mgawanyo wa mapato ambao hauwezi kuleta matatizo.
Naamini kabisa kama lengo la Cecafa ni kuinua kiwango cha soka katika ukanda huu basi ijiangalie ni jinsi gani inaweka mambo haya ya mapato sawa kabla ya mashindano. Na pia ufike wakati busara itawale tamaa zetu za kupenda fedha miongoni mwa viongozi wa vilabu. Yanga imetutia aibu kama Taifa manake hainiingii akilini viongozi kutokuleta timu uwanjani. Utafikiri hayo mamilioni waliyokuwa wanayalilia wangeyatumia vizuri. Hii ni timu inang’ang’ania mapato makubwa lakini huoni wanazifanyia nini. Ni timu ambayo ni kongwe lakini haina hata uwanja wa kisasa wa kufanya mazoezi ama hata ofisi za kisasa ambazo kama klabu ingepaswa ioneshe mfano.
Tatizo la Yanga karibu lifanane na lile la Simba kujitoa kombe la Tusker eti mgao lilikuwa tatizo. Mimi huwa nashangaa hawa viongozi wa vilabu vyetu hivi kwanini wanadai mafedha lakini hatuyaoni yakitumika kuleta tija kwenye vilabu? Hebu angalia Simba nayo hawana hata kiwanja cha mazoezi. Hivi klabu kama Simba ikiendelea kutembelea vilabu kama vile Sport Club Villa pale Kampala wataamini watakachokikuta pale kwenye kiwanja chake cha Villa Park? Nasema ni bora sasa tuwaulize wote waliowahi kuwa viongozi wa vilabu hivi wamevifanyia nini vilabu hivi? Kama sio ufisadi wa kimafia mafia tu hamna lingine zaidi ya kushibisha matumbo yao.
Tatizo la Tanzania ni kuwa wengi wa viongozi wa vilabu wawe ni wachezaji wa zamani ama hata mashabiki uchwara, hakuna kabisa utashi wa maendeleo ya jumla bali ni ubinafsi mtindo mmoja.
Kwa haya yalitokea kwa Yanga ni kielelezo tu cha jinsi gani nchi yetu imeporomoka kimaadili na tumbo zimewekwa mbele kuliko kitu kingine. Katika hali hiyo tusitegemee mpira kuendelea kirahisi hasa kutokea timu za Simba na Yanga. Tuanze kwenda mikoani na tuliimarishe soka la mikoani kwanza na haya mambo ya migao yatakwisha tu.
Mwisho, naamini Yanga lazima ipewe adhabu kubwa iwe ni fundisho. Na TFF iache haya mambo ya kuzilea hizi timu kubwa lakini zisizokuwa na lolote la kuigwa katika maendeleo ya soka la nchi yetu. Kwa vyovyot e vile yaliyotokea ni hii mazoea ya TFF kuziona Yanga na Simba kama Mungu na kuzitumia kama nguzo kuu ya kupata fedha. Kwa maana hiyo, kwasababu fedha ni muhimu kuliko chochote kwa TFF na vilabu hivi basi ndio maana haya yametokea. Inahitajika utendaji kazi wa kisasa (professionalism) ili tufike kisoka wenzetu walikofika.
Tuesday, July 29, 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment