Thursday, June 26, 2008

TAIFA STARS HAIKUWA NZURI SANA (Not good enough)

Najaribu kumfikiria na kumchambua Marcio Maximo pamoja na timu yake napata shida sana kuamua je tatizo ni kocha ama wachezaji? Nikitaka niwapongeze kwa jinsi walivyokufa kiume nashindwa manake naweza sema kuwa katika mechi zao mbili dhidi ya Cameroon kitu pekee walichofanya ni kuwabana Cameroon na kuzuia ama kuharibu mtiririko mziima wa uchezaji wa Cameroon.
Sikuona kama timu ya Taifa Stars ilikuwa na uchezaji wenye mfumo hasa. Kwa maana nyingine sidhani kwa uchezaji wa aina ile ningekuwa na fikira za timu kufuzu kwenda Angola ama Afrika Kusini. Timu yetu haina kiungo mchezeshaji (playmaker) na hivyo timu yetu imejengwa kwa kuegemea ulinzi tu. Tunacheza tukijitahidi tusifungwe wala hatushambulii kabisa na matokeo yake tunashindwa hata kupata ushindi wa mechi ndogo kama Mauritius. Ndio maana hadi leo hatuna mchezaji nyota hasa kwani huwezi kusikia kama fulani hayupo basi leo timu itapwaya. Ni lazima timu iwe na mchezaji ama wachezaji wachache mahiri ambao ni roho ya timu ndio tunaweza kufanikiwa ninaamini.

Hili nadhani ni tatizo la kitaifa manake hata nikitizama jinsi timu zetu za ligi kuu zinavyocheza mara nyingi huoni kama kuna mfumo ama kuna uchezaji wa mbinu za kupanga mashambulizi. Na mara nyingi si timu ya Taifa Stars tu bali hata Simba na Yanga pamoja na timu zote za Mikoa ambazo zilishiriki mashindano ya Taifa Cup sikuona mfumo kabisa.
Tunachoweza tu ni kulinda lango lakini unapoanzia idara ya kiungo cha ushambuliaji na ushambuliaji ni bure kabisa. Ni katika mtizamo huu nina wasiwasi hata tukimlaumu Maximo na akina Tinoco bado tunabaki tukijiuliza hivi Makocha wa vilabu vyetu wameshindwa nini? Kwanini wachezaji wetu si wabunifu? Hata pale timu inapokuwa nyuma kimchezo bado hatuoni mchezaji hata akijaribu basi kupambana kwa juhudi binafsi. Ni hatari sana kwa uchezaji wa aina hii kwani inatia shaka kama kweli wachezaji wetu wana moyo wanapoichezea timu ya Taifa.
Soka ya Tanzania inachezwa na magazeti sana kwa kuwadanganya wachezaji wetu kuwa wapo juu. Nina mifano miwili hapa: Ngassa kapigiwa sana debe kuwa ni mahiri lakini alipopewa nafasi dhidi ya Cameroon imedhihirika kuwa bado ana safari ndefu sana hasa kimbinu na nguvu. Hana nguvu kabisa na katika mechi dhidi ya Cameroon mara nyingi alishindwa kujua acheze namna gani dhidi ya wachezaji wenye maumbo makubwa. Sidhani kama ilikuwa ni busara kwake kucheza karibu sana na mpinzani ukizingatia ana kasi lakini mara nyingi alikuwa anakaa na mpira kumsubiri adui nah ii ilimshinda.

Mfano wa pili ni kuhusu jinsi mabeki wetu wa pembeni wanavyocheza: sipendi kabisa uchezaji wa kizamani ambao nimeushuhudia katika mechi zote hadi sasa. Beki kama Nsajigwa ana uwezo mkubwa wa kupanda mbele na kushambulia. Nadhani ukizingatia tuna beki mwingine mzuri wa kulia …………… basi ingekuwa vyema upande wa kulia tuwatumie wote upande wa kulia na ninaamini mambo yangekuwa mazuri.
Kitu kingine ambacho naamini kwa timu changa na isiyo na uzoefu kama yetu ingefaa ikizingatie basi ni upigaji wa mashuti ya mbali. Wachezaji wetu hawapigi mashuti ya mbali kabisa wanataka kupenya ngome ya adui wakati hawana uwezo wa kupasiana na kubadilishana mpira ipasavyo.
Si kupasiana tu ila kuna upigaji vichwa na matumizi ya kifua katika kumiliki mpira. Mara nyingi wachezaji wetu wanaonekana kabisa hawajui kupiga vichwa wala kutumia kifua katika kucheza mpira. Mpira wa juu wowote utaona wanaucheza kwa woga na mara nyingi mtu akipiga kichwa anapeleka kwa adui. Nadhani kwa makocha wa vilabu vyetu ni lazima hili lifanyiwe kazi manake ni balaa kwa wachezaji wa kitanzania. Hata hii michuano ya Coca Cola kwa vijana nimeona hili ni tatizo kabisa. Inaonekana walimu wetu hawazingatii mambo kama haya ambayo ni muhimu sana kwa mchezaji kuweza kumudu mechi zenye wachezaji wa kiwango cha wale wa kulipwa Ulaya.
Jambo lingine ni kuwa sasa umefika wakati tuangalie mfumo wa waamuzi wetu kupenda virushwa kwani ni wazi wachezaji wetu hasa wa vilabu vikubwa wamezoea kubebwa na inawawia vigumu kuweza kumudu mechi za kimataifa ambazo ni mara chache mchezo mchafu kuwezekana.

Yapo ambayo yanatakiwa yafanyike kwani kila kitu kinawezekana. Mosi ni vyema Ligi Kuu iimarishwe kwa kuzingatia viwango (standards) na kutoruhusu mizengwe na upendeleaji wa mara kwa mara kwa vilabu vikubwa; hii haisaidii sana soka letu. Pili, TFF ipanue wigo wa kupata wachezaji mahiri kwa kuhakikisha kunakuwa na Ligi Daraja La Kwanza ambayo itaongeza wigo wa kupata wachezaji kwenye timu ya Taifa. Hii itasaidia hasa kuwanyanyua wachezaji wenye vipaji adimu mikoani ambako ni vigumu kuweza kuonwa tu na vilabu vya ligi kuu.
Labda niseme tu sikutarajia kama tungefuzu hasa pale tulipopoteza mchezo dhidi ya Mauritius hapa nyumbani. Hatukustahili sare kabisa na nadhani umefika wakati wachezaji wetu wajue kuwa mchezo wa nyumbani ni lazima washinde; na timu yeyote inayoshindwa kupata ushindi nyumbani basi imepoteza nafasi ya kufuzu mashindano. Ndio maana baada ya mechi ile nilijua basi tena tumekwisha. Lazima wachezaji wetu waige kwa majirani zetu Kenya, Uganda na Rwanda jinsi wanavyohakikisha hawashindwi mechi za nyumbani. Pale tu tutakapoweza kushinda mechi za nyumbani basi tutakuwa na nafasi ya kufuzu mashindano yeyote yale.

Mwisho kabisa najiuliza hivi kweli wachezaji wetu huwa wanatizama mechi za ligi za Ulaya na kufuatilia kwa dhati? Inaonekana kabisa bado hata masuala madogo madogo ya kiuchezaji hasa mbinu kwao ni taabu sana. Mara nyingi naangalia jinsi ambavyo wanavyoshindwa hata kujipanga wakati wa kupiga mipira ya adhabu inanikera sana. Natoa rai kwa wachezaji wetu kama kweli wanaupenda mpira basi wafuatilie nini kinafanywa na wenzao wa huko Ulaya.
Nimalizie kwa kuitakia Taifa Stars iweze kuifunga Sudan mwezi wa September ili angalau basi tuweze kufuzu kwenda kwenye fainali za wachezaji wasio wa kulipwa Ulaya. Hii itakuwa ni hatua moja mbele kwa wanasoka wa kizazi cha leo na ambayo itatusaidia kupata hata nyota wachache watakaouzwa huko Ulaya. Manake bila kuwa na wachezaji wa kulipwa Ulaya tutaendelea kuwa wasindikizaji tu. Wenzetu majirani Uganda wanafanya vizuri tu.
Unaweza kuona ndio maana kwa sasa hadi raundi hii ya nne inamalizika msimamo wa kundi letu unaonesha jinsi tulivyo taabani kwa matokeo ya mechi tulizokwishacheza:
01-02/06/08: Cameroon 2-0 Cape Verde 01-02/06/08: Tanzania 1-1 Mauritius
06-08/06/08: Cape Verde 1-0 Tanzania 06-08/06/08: Mauritius 0-3 Cameroon
13-15/06/08: Tanzania 0-0 Cameroon 13-15/06/08: Mauritius 0-1 Cape Verde
20-22/06/08: Cameroon 2-1 Tanzania 20-22/06/08: Cape Verde 3-1 Mauritius
Msimamo mzima wa makundi yote waweza kuusoma jinsi ulivyo hapa hadi raundi ya nne.

No comments: