Hatimaye michuano ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2010 huko Afrika ya Kusini pamoja na zile za Mataifa ya Afrika kule Angola zimefikia raundi ya pili. Kampeni za Tanzania, Taifa Stars zimeendelea kusuasua kama nilivyobashiri kuwa itakuwa ni mechi ngumu sana. Hawa mabwana wa Cape Verde wameifunga Taifa Stars kwa bao moja bila majibu.
Cape Verde nawakumbuka vizuri walicheza na Harambee Stars katika harakati za kufuzu michuano iliyopita na waliipa shida sana timu ya Kenya katika mechi ya marudiano. Hivyo nilitaraji tutapata taabu sana. Sidhani ni wakati wa kumlaumu mtu yeyote kwani nilifuatilia mechi ile redioni na ninaweza kusema tumefikia ukomo wetu kama Taifa. Aina ya wachezaji tulionao hata aje Scolari ama Erickson hapa bongo, ni kwamba tuna safari ndefu sana katika soka. Na kwasababu hatutaki kuamini ukweli huu, basi hatutaendelea kisoka kabisa.
HATUNA ‘QUALITY PLAYERS’
Kwanini ninasema hivi? Mosi, Kocha Marcio Maximo anapigiwa kelele sana eti hana uwezo na ndio chanzo cha kufungwa kwetu. Mimi tangu aje nchini kwetu sikubaliani na hoja za wanaojiita wadau wa soka la bongo hata kidogo. Naamini maamuzi mengi ya Maximo ni kitaalam zaidi na ambayo kwa wengi wa watanzania hawayajui wala hawayataki. Watanzania wengi wanapenda mambo ya kienyejienyeji yasiyozingatia taratibu za fani husika. Kwa mfano, kuna wachezaji ambao wanapigiwa upatu waitwe kwenye timu hii lakini ukitizama kwa kina unaona kuna msukumo wa unazi wa “usimba na uyanga” katika madai ya wadau wengi.
Pili, suala la nidhamu ya wachezaji wetu ni tatizo la elimu miongoni mwao. Kwa uelewa wangu wa soka la bongo, wachezaji wetu wengi ni wale ambao ama wameacha shule na kujikita kwenye soka kama njia fupi kufikia mafanikio ya kimaisha. Wengine walifukuzwa shule kwa utovu wa nidhamu na wengi wao ni watumiaji wa vilevi mbalimbali ambavyo ni kinyume na maadili ya kimichezo. Kwa ujumla kandanda la bongo limejaa makapi kutoka katika fani nyingine na ndio hapa ninapoona uozo wa wachezaji wetu na sishangai hasa wachezaji wanapofukuzwa kambini ama wengine wanapokataliwa kuitwa timu ya Maximo licha ya kelele za wadau wengi ambao hata wao hawajui kanuni za soka kwa undani.
Tatu, kuna suala la kuwa je tuna wachezaji nyota Tanzania? Kwangu nadhani niseme hatuna na bado tuko kwenye mwanzo wa kuwavumbua. Hebu tujiulize maswali kadhaa: Je kwanini hatuna wachezaji wanaocheza soka la kulipwa Ulaya? Kama kwele vilabu vyetu kila mwaka vimeshiriki mashindano ya Afrika na hata timu yetu ya Taifa imeshiriki michuano ya kimataifa inakuwaje hatuvutii mawakala wa timu za nje ambao huwa wanakuwepo kutafuta nyota wa kuwanunua? Jibu ni kuwa wale tunaodhani ni nyota bado si nyota kwa viwango na vigezo vya kimpira vya kileo. Sisi tunawapima kwa vigezo vya kitanzania basi tunawaona kama malaika! Masikini wakubwa wa mawazo na upeo wa soka ndio ugonjwa unaotukabili haswa.
Nne, ningependa nitoe rai kwa watanzania kuwa tuache njozi na kufuata hisia zaidi ya hali halisi na kukubali ukweli. Nasema hivi kwani nina mifano kadhaa kuonesha jinsi soka yetu inavyoegemea zaidi hisia (fantasy) kuliko uhalisia. Nitoe mfano wa wachezaji wawili: Juma Kaseja na Athuman Machupa. Haipingiki kabisa kuwa Kaseja ni kipa bora kabisa hapa nchini na ni vigumu kumwelewa Maximo kutokumtumia wala kumwita timu ya Taifa. Lakini huwa najiuliza kitu kimoja kumhusu Kaseja: Kwanini kwa muda wote ambao amecheza soka hapa nchini hasa mechi nyingi za kimataifa inakuwaje hajawahi hata kuitwa kufanya majaribio ya soka la kulipwa katika vilabu vikubwa vya Afrika ya Kaskazini ama vile vya Afrika ya Kusini?
Katika mechi alizocheza alipata nafasi tosha kabisa kuonesha uwezo wake katika nchi mbalimbali lakini bado hakwenda japo hata hapo Rwanda ama Uganda. Hii inanifanya nimwone Kaseja kama mchezaji mahiri lakini kiviwango hapitani ama hapishani sana na wanasoka wengine ambao ni magolikipa hapa Tanzania. Yaani namaanisha umahiri wake si ule tunaoweza kuuita usio kifani. Na hili Maximo analijua ndio maana haangaiki labda.
Ukija kwa Athuman Machupa, huyu alipigiwa kelele sana eti aitwe time ya taifa na aliitwa na akashindwa kumthibitishia Maximo amwite tena. Ila kwangu kuna wakati nilisikia alikuwa nchini Uingereza akifanya majaribio ya soka kule nikasema sasa tutapata nyota. Lakini kwa mshangao nikasikia yuko Rwanda leo yuko Simba na mara nyingine yuko Mchangani. Je kama sisi tunamwona kama nyota lakini Uingereza tena madaraja ya chini kashindwa kufuzu majaribio, hapo tutaendelea kumpigia Maximo makelele amwite eti kwasababu ya hisia tu?
Mifano hiyo miwili ni kujaribu kuonesha jinsi gani soka letu bado liko usingizini na tunahitaji muda mrefu ili kuweza kufika pale tutakako. Tukiacha kuheshimu hisia basi tutafika lakini pale tutakapomfukuza Maximo na kufikiri tukirejesha kuendesha soka yetu kienyejienyeji kamwe hatutakaa tufike.
MATUMAINI YA KUFUZU YAPO?
Ni wazi kama mtanzania yeyote anafikiri tunaweza kufuzu kwenda Angola ama Afrika ya Kusini basi huyo hajui soka. Ili timu ifuzu kwenda kombe la dunia ni lazima nchi iwe na angalau klabu moja yenye mafanikio kisoka katika michuano ya kimataifa ambayo ndio itakayokuwa roho ya timu ya Taifa. Chukulia mifano ya nchi kama Angola, Tunisia, Misri, Libya na hata Benin ambazo wachezaji wake wengi ni wa ndani ya nchi. Huwezi kufuzu michuano mikubwa kama uendeshaji wa vilabu ni wa kienyeji ukifanyika katika vilabu vya pombe na kahawa chini ya watu wanaojiita marafiki wa klabu.
Nimalizie kusema tu kuwa kwa matokeo ya Cape Verde, basi naamini timu yetu imepoteza mwelekeo na sidhani kama tunaweza kufuzu labda tu tuifunge Cameroon hapa nyumbani wikendi ijayo na tuhakikishe hatupotezi tena wala kutoa sare mechi zijazo. Kinyume na hapo, timu ya Maximo kwa sasa ni kuendelea kulea kufundisha wachezaji wetu namna ya kusakata gozi. Ufike wakati wadau wa soka wafungue macho na kuona mbele. Tatizo si kocha wala upangaji wa timu, nadhani hatuna wachezaji wa kucheza soka la kiwango cha wapinzani wetu. Ukweli ni kuwa tujiulize kwanini wachezaji wetu nyota wanaishia Uarabuni kule ambako wanakwenda wachezaji wastaafu wa soka toka Ulaya?
Natoa rai, tusitafute mchawi hapa ila turidhike na matokeo na tuhangaikie zaidi timu za vijana kwani kwa sasa kazi ya Maximo ni kuvumbua vipaji kwa ajili ya baadaye sana. Tuangalie uendeshaji wa mchezo huu ngazi za mikoa na wilaya ndiko kwa kuanzia. Mungu Ibariki Tanzania.
Sunday, June 8, 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment