Hatimaye michuano kuwania nafasi ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2010 huko Afrika ya Kusini zimeanza. Hizi ni fainali za kufuzu pia kwa kombe la Mataifa ya Afrika huko Angola hapo mwaka 2010. Hii ni makala ya kwanza ya ufunguzi wa blog hii ambayo itajikita katika masuala ya soka kwa ujumla wake. Nitachambua fainali hizi kwa undani hasa.
Kwa maana hiyo Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars ilianza michuano hii kwa balaa kwani ilitoka sare na Timu ya Mauritius ambayo ilikuwa ni dhaifu sana. Wakati naandika waraka wa leo ndio timu imeondoka alfajiri ya leo kuelekea huko Cape Verde.
Katika mchezo ule kiwango cha uchezaji kilikuwa cha chini sana hasa katika kiungo cha ushambuliaji kwani inaonekana wazi kabisa hatuna mchezaji wa kuchezesha timu na kugawa pasi za mwisho kwa wafungaji. Wafungaji wanapewa pasi fyongo mara zote na inakuwa vigumu kufunga kwa urahisi. Ni lazima Maximo atafute wachezaji wa aina ya akina Messi ama Fabregas ili kuweza kuwatisha walinzi wa timu pinzani kurahisisha upenyezaji wa mipira yenye tija.
Ilikuwa ni mechi ya 25 kwa Maximo kama kocha akiwa na rekodi ya kupoteza mechi tano na kushinda mechi na kutoka sare 11. Ni rekodi nzuri. Katika mechi hii ya kwanza kwa michuano Maximo alitumia wachezaji wafuatao: Ivo Mapunda, Fred Mbuna, Maftah, Sallim Sued, Harob Canavaro, Godifrey Bonny, Henry, Emanuel Gabriel, Ulimboka, Jerry Tegete, Kigi Makassy, Athuman Idd na Nizar Khalfan.
Sijui atabadilishaje timu yake mechi ijayo tusubiri tuone.
Binafsi naamini kama kuteleza basi hapa ndio penyewe japo naamini ili tujisahihishe ni lazima tushinde mechi ya Cameroon hapa nyumbani wiki mbili zijazo na pia mechi ya Cape Verde wikiend hii. Tusiposhinda mechi hizi mbili basi kufuzu tusahau kabisa kwani ili tufuzu lazima tuwafunge Cameroon.
Kushindwa kuifunga Mauritius kulisababishwa na aina ya wachezaji tulionao hapa Tanzania. Naamini wachezaji wetu hawaangalii mipira mikubwa katika televisheni na kama wanatizama basi wanatizama picha na huwa hawasikilizi maoni ya watangazaji (commentaries) kwani huwa yanakuwa yamesheheni ushauri wa kitaalam ambao kwa vijana wetu kama wakifuatilia basi watafika mbali sana.
Haiwezekani unacheza nyumbani alafu unashindwa kufunga magoli hasa ukizingatia upinzani ulicheza na wachezaji kumi kwa muda mrefu. Timu yetu wachezaji wengi hawatumii akili kabisa. Sikufurahishwa na upigaji wa krosi nyingi ambazo hazikuwa zinalengwa kwa wafungaji bali kupiga tu kwa nguvu ili mfungaji autafute kitu ambacho naamini ni kigumu sana.
Maoni yangu ni kwamba Taifa Stars haijui aina ya uchezaji ya watu kama David Beckham ama Fabregas ambao upigaji wao wa pasi unakuwa ni kupeleka mpira kwa mtu na si kuupiga tu kwa nguvu ili mtu akutane nao. Mpira wa krosi sharti uwe umelengwa kwa mtu (intended to) na si kujipigia tu. Kama hatutaacha aina hii ya uchezaji basi tusijidanganye hata aje nani hapa bongo tutakuwa tunasikitika sana kila michuano.
Katika fainali hizi majirani zetu Kenya watacheza na Guinea chini ya Paschal Feundono wakati Uganda iko Benin ikicheza huko.
Nimalizie kwa kusema kuwa mechi ya wikiendi hii itakuwa ngumu kwani hawa Cape Verde si timu ya kubeza hata kidogo. Ni timu ambayo iliihangaisha sana Kenya katika michuano iliyopita na ina kiwango cha juu cha soka. Ninaamini kama TFF na akina Maximo wana utashi wa dhati na kazi yao watakuwa wameshawatizama hawa Cape Verde kupitia mikanda ya mechi zao walipocheza na Kenya katika fainali za Mataifa ya Afrika zilizopita kwani ni rahisi kuzipata kutoka kwa jirani zetu.
Mwisho niitakie Taifa Stars ushindi kwa mechi ya kesho.
Thursday, June 5, 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment